Neno la Ukaribisho
Karibu kwenye Tovuti rasmi ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo. Taasisi iko katika Manispaa ya Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam.
Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo ni Taasisi pekee inayotoa mafunzo kwa wahitimu wa sheria ambao wanatamani kuwa wataalamu wa sheria katika utumishi wa umma au kazi binafsi nchini Tanzania Bara. Baada ya kuhitimu shahada ya kwanza katika sheria kwenye chuo kikuu kinachotambulika, wanafunzi huhudhuria mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo ambayo ni mahsusi kuwaandaa kwa ajili ya kusajiliwa kama Mawakili au kufanya kazi kama wanasheria kwenye utumishi wa umma.
Taasisi ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge, Sheria Namba. 5 ya mwaka 2007 na ilianza kufanya kazi rasmi tarehe 2 Mei, 2008. Hii ilikuwa ni hatua muhimu kwenye kuboresha ujuzi wa vitendo kwa wanasheria nchini. Kabla ya kuanzishwa kwa Taasisi, wanasheria walikuwa wanapata ujuzi wa vitendo kupitia mafunzo kazini ambayo yanatolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Baadae baadhi ya vyuo viliaanzisha mfumo wa mafunzo ya ujuzi kwa vitendo kwa wanafunzi wa sheria. Mifumo hii ndiyo kwa sasa imechukuliwa na Programu ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo inayotolewa na Taasisi. Taasisi iko chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Pamoja na kutoa mafunzo kwa vitendo, Taasisi inatoa kozi ya Astashahada ya Sheria (NTA ngazi 4), pia inatoa huduma mbalimbali ikiwemo msaada wa kisheria (Legal Aid), ushauri wa kisheria, inatoa huduma ya kozi fupi na semina, inafanya utafiti wa sheria, inajenga mahusiano na vyuo na taasisi mbalimbali nchini na kimataifa.
Udhibiti na usimamizi wa Taasisi uko chini ya Bodi ya Uongozi ambayo wajumbe wake wameelezwa kwenye sheria. Kazi za kila siku za Taasisi zinasimamiwa na Mkuu wa Taasisi ambae ndie Mtendaji Mkuu na Afisa Masuuli wa Taasisi.
Imeandaliwa na
Prof. Sist J. Mramba
Kaimu Mkuu wa Taasisi
Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania