KATIBU MKUU MASWI AIPA KONGOLE LST
KATIBU MKUU MASWI AIPA KONGOLE LST
09 Apr, 2025

KATIBU MKUU MASWI AIPONGEZA LST KWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Maswi ameipongeza Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi katika kutekeleza majukumu yake.
Bw. Maswi aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo lililofanyika kwa siku mbili mkoani humo.
"Mimi kama Katibu Mkuu wenu nafarijika kuona Taasisi hii inafanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa weledi, hongereni sana." Alisema.
Pia Bw. Maswi aliwapongeza viongozi wa LST na Chama cha Wafanyakazi kwa kuzingatia umuhimu wa uwepo wa Baraza sambamba na kufuata sheria, kanuni na taratibu ambazo zinaelekeza Taasisi, Wizara na Mashirika ya Umma kuunda Mabaraza ya Wafanyakazi na kuwa na vikao viwili kwa mwaka.
"Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu sana katika kutekeleza dhana nzima ya utawala bora kwa kuwa linatoa fursa ya ushirikishwaji wa wafanyakazi kupitia chama chao na wale waliochagulia kupitia idara ama vitengo vyao kushiriki katika majadiliano ya pamoja na Menejementi ya Taasisi na kuweza kutoa maoni ama mapendekezo. Majadiliano haya hulenga katika kuboresha ustawi wa Taasisi pamoja na watumishi." Alibainisha.
Sambamba na hayo, Bw. Maswi alitoa rai kwa Watumishi wa LST kuendelea kufanya kazi kwa juhudi kwa kuwa Taasisi hiyo ni ya kitaaluma hivyo utendaji wake unapaswa kuzingatia ubora, nidhamu na weledi wa hali ya juu ili kupata tija inayokusudiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Sist Mramba alimshukuru Bw. Maswi pamoja na Watendaji wengine wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana bega kwa bega na LST katika kuhakikisha wanaboresha huduma na kuimarisha ustawi wa Taasisi na watumishi wake.
Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania ilifanya kikao cha pili cha Baraza la Wafanyakazi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kuanzia tarehe 3 hadi 4 Aprili, 2025.