Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST)

lst Logo
Naibu Waziri Sagini Atembelea LST
07 Jun, 2024
Naibu Waziri Sagini Atembelea LST

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini ametoa rai kwa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), kuvishauri vyuo vinavyozalisha wasomi wa sheria nchini kuzuia ufaulu wa kukariri badala yake wafaulu kwa kuelewa masomo.

Sagini aliyasema hayo tarehe 29 Mei, 2024 alipotembelea LST na kuzungumza na uongozi pamoja na wafanyakazi kuhusu masuala mbalimbali ya kikazi, taaluma na mahusiano kazini.Alisema hulka ya wanafunzi kukariri na kufaulu mitihani inawapa tabu wanapofika LST kuandaliwa kwa ajili ya kuwa mawakili kwa sababu mafunzo ya kuandaa mawakili ni tofauti na masomo wanayosoma chuoni.

 

Aidha, Sagini alisema ili mwanafunzi aweze kufaulu mafunzo ya uwakili ni lazima ajiunge na LST akiwa na ombwe kichwani la kujifunza vitu vipya katika mazingira ya kazini. Vilevile, Sagini aliitaka LST kuongeza bidii katika kuzalisha wataalamu wengi wa sheria ili watumike kutoa ushauri wa kisheria kote nchini ili wananchi waelewe kuwa mamlaka inayotoa haki ni Mahakama pekee.

Wakati huohuo, Sagini aliwataka maofisa wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa weledi katika kuwahudumia wananchi. Kuhusu mafunzo ya Wasaidizi wa Kisheria yanayotolewa na LST, Mhe. Sagini aliitaka LST kuhakikisha inaendelea kujitangaza katika vyombo vya habari ili wananchi wapate kufahamu mafunzo hayo.

Naye Kaimu Mkuu wa LST, Prof. Sist Mramba alisema taasisi imefanikiwa kuanzisha program mpya ya Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) ambayo ni program ya kwanza kuanzishwa Tanzania kwa ngazi ya cheti.

 

Alisema program hiyo imeanza na wanafunzi 15 na wote walihitimu na kutunukiwa vyeti vyao huku ikiendelea kushirikiana na wadau wengine likiwemo Baraza la Taifa la Mafunzo ya Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (NACTVET) ili kupata ithibati kwa program zingine. Alisema LST pia imefanikiwa kupitia upya mtaala wake na kufanya marekebisho na mtaala huo utaanza kutumika Julai 2024.

Aidha alisema taasisi mpaka sasa imesajili wanafunzi 17,782 waliopata mafunzo ya Stashahada ya Uzamili ya Sheria kwa Vitendo (Post Graduate Diploma in Legal Practice) na kati yao wanafunzi 8,999 sawa na asilimisa 56 walifaulu.

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
https://saris.lst.ac.tz/Registrations

" >